Tuesday, 6 February 2018

SARATANI DALILI ZAKE KUCHUKUA MIAKA 5 HADI 10


TAASISI ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), imewataka Watanzania kujijengea utamaduni wa kupima saratani kila mara kwa sababu ugonjwa huo hukaa mwilini kati ya miaka mitano hadi 10 kabla ya dalili kujitokeza.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka ORCI, Dk. Crispin Kagesa alisema upimaji wa afya mara kwa mara ndio utakaomwezesha Mtanzania kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema endapo watu watapima afya na kugundulika mapema ni rahisi kutibiwa na kupona kuliko kusubiri ugonjwa kufikia hatua ya mwisho.

Wakati Dk. Kagesa akisema hayo, takwimu zinaonyesha kila mwaka watu 50,000 hupatwa na saratani nchini.

“Ugonjwa unakaa mwilini muda mrefu na kama mtu hatajijengea tabia ya kuchunguza afya yake mara kwa mara, dalili zitajitokeza na bila kufahamu kama ni dalili za saratani hadi atakapobainika anayo, ugonjwa unakuwa umefika hatua mbaya,” alisema.  

Dk. Kagesa alisema wapo wanaopata mabadiliko kwenye miili yao ambayo hayaonekani kwa macho hivyo kama hawatapima husababisha tatizo kugundulika likiwa katika hatua mbaya.

“Kama mtu atapata mabadiliko mwilini mfano uvimbe kwenye shingo ya kizazi au utumbo, sio rahisi kujigundua mapema kama hatajijengea tabia ya kupima afya yake mara kwa mara," alisema.

"Dalili za ugonjwa zinazoambatana na maumivu ndizo zinaweza kumfanya mtu kukimbilia hospitali.”

Alisema yawezekana mtu akajiona yupo salama kiafya lakini kumbe mwilini ana tatizo ndio maana inashauriwa kupima afya mara kwa mara.

“Saratani inatibika, hivyo usichelewe, wahi upate uchunguzi na matibabu, takwimu zinaonyesha wagonjwa wengi wamekuwa wakifika hospitali wakiwa katika hatua ya mwisho ya ugonjwa,” alisema.

Dk. Kagesa alitaja mambo yanayochangia kupata saratani kuwa ni pamoja na maambukizi ya virusi, bakteria au parasaiti.

“Kuwa na mfumo usiofaa kimaisha kama utumiaji wa tumbaku, pombe kupita kiasi, kula chakula kisichofaa, kutokufanya mazoezi na unene kupita kiasi,” alisema.

Alitaja sababu nyingine kuwa athari za mazingira kama mionzi, kemikali za maji na gesi pamoja na historia katika familia kutokana na mabadiliko ya vinasaba.


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment