Wednesday, 7 February 2018

PROF. KABUDI ASEMA HAKUNA MGONGANO WA KATIBA BARA NA VISIWANI


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema hakuna mgongano mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko la kero za Muungano.

Prof. Kabudi aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wingwi (CUF), Juma Kombo Hamad, ambaye alitaka kujua ni lini serikali ya Muungano italeta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto zilizomo ndani ya katiba hizo.

Alisema kumekuwapo na mgongano mkubwa wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar unaosababisha ongezeko kubwa la kero za Muungano na mgongano wa kimamlaka baina ya serikali mbili.

Prof.Kabudi alisema hakuna mgongano wa kimamlaka baina ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

“Katiba ya Jamhuri ya Tanzania imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia tafsiri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake inayobishaniwa kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema Waziri huyo.

Aidha, alisema hadi sasa hakuna upande wowote baina ya serikali hizo mbili ambao unatafsiri tofauti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano au utekelezaji wake.

Alisema kwa kuwa hakuna mgongano wa Katiba kati ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar, serikali haina sababu ya kuleta mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba ili kuondoa changamoto ambayo haipo.

Katika swali lake la nyongeza, Hamad alisema katika siku za karibuni kupitia vyombo vya habari ameona Rais John Magufuli akitoa maagizo kwa Waziri wa Zanzibar, na kuhoji kikatiba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana mamlaka ya kikatiba kutoa maagizo kwa waziri huyo.

 Prof.Kabudi alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka yote ya mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi huru.

“Kwa hiyo katika mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mkuu wa nchi ni mmoja tu, ni Rais Magufuli na yeye peke yake ndiye Amri Jeshi, hakuna mtu yeyote wa kuamuru majeshi ya Tanzania isipokuwa Rais wa Jamhuri kwa sababu yeye peke yake ndiye mkuu wa nchi,” alisema.

Aliongeza “Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye heshima na hadhi ya urais kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano yanayohusu Zanzibar, lakini pia ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi yake hiyo.”

Aidha alisema kwa kuzingatia usawa wa wabia wa Muungano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatoka Tanzania Bara na Makamu wake atatoka Tanzania Zanzibar na ikiwa Rais atatoka Zanzibar, makamu atatoka Tanzania Bara.


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment