Monday, 12 February 2018

Mbunge amwomba Rais Magufuli matibabu kupitia mitandao


MBUNGE mstaafu wa Kilombero (CCM), Abdul Mteketa, ambaye aliomba msaada wa matibabu ya upasuaji wa magoti kwa Rais John Magufuli kupitia mitandoa ya kijamii, amesafirishwa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutibiwa.

Jumamosi iliyopita, Mteketa alirekodi ujumbe wa video na kuuweka kwenye mitandao ya kijamii akimwomba Rais Magufuli amsaidie matibabu kwani hali yake kiuchumi ni mbaya.

Mteketa aliyetumikia jimbo la Kilombero kwa miaka mitano baada ya kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, alishindwa kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM kwa ajili ya kutetea kiti hicho 2015.

Katika ujumbe wa video alioutuma Jumamosi, Mbunge huyo mstaafu alimweleza Rais Magufuli kuwa hali yake ya kiafya ni mbaya na kwamba amekuwa akibebwa kwenda maliwatoni na kuogeshwa.

"Mheshimiwa Rais John Magufuli, mimi ni Abdul Mteketa, Mbunge mstaafu wa Kilombero nipo hapa mbele yako kwa sababu nimejitahidi miaka yote kukufikia lakini nimeshindwa tangu uingie madarakani," alisema na kueleza zaidi:

"Hali yangu kiafya ni mbaya kama unavyoniona, nabebwa kwenda chooni, naogeshwa, kila kitu nategemea msaada wa mtu. Nimejitibu kwa mwaka mzima sasa lakini bila mafanikio.

"Nimeenda kwa madaktari wameniambia tatizo ni magoti, kwanza nimeumwa mguu huu madonda kila sehemu yamepona, magoti yangu yanatakiwa kufanyiwa upasuaji."

Siku iliyofuata, Mteketa aliweka tena ujumbe mwingine wakati akiwa kwenye gari la kubeba wagonjwa baada ya Rais Magufuli kumsaidia ambamo anamshukuru kiongozi huyo wa taifa.

Mteketa anasema katika ujumbe huo kuwa baada ya Rais Magufuli kuona ujumbe wake wa video aliyoituma kwenye mitandao ya kijamii Jumamosi, alichukua hatua ya kumsaidia.

"Jana (Jumamosi) nilituma ujumbe wa video ya hali yangu kuwa mbaya, niliyompelekea Rais, alipoiona leo (Jumapili) amechukua hatua; amenitumia gari la wagonjwa ambalo sasa hivi nipo ndani napelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili," anasema.

"Nakushukuru sana Rais, Chama cha Mapinduzi CCM na Watanzania waliopeleka ujumbe wa video yangu mpaka zimemfikia Rais. Naomba mniombee."


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment