Tuesday, 6 February 2018

BUNGE LAITAKA SERIKALI KUISAIDIA TANESCO KULIPA MADENI YA MABILIONI


BUNGE limeitaka serikali kulisaidia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kulipa madeni ya mabilioni ya shilingi yanayolikabili kiasi cha kulifanya lishindwe kujiendesha kwa ufanisi.

Agizo hilo lilitolewa bungeni mjini hapa jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Deogratius Ngalawa, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati yake kwa kipindi cha Januari 2017 hadi Januari, 2018.

Alibainisha kuwa hadi Desemba 31, shirika lilikuwa linawadai wateja wake ambao ni serikali na taasisi zake pamoja na wateja binafsi Sh. bilioni 277.4. Wateja binafsi wanadaiwa Sh. bilioni 83.8 wakati serikali na taasisi zake likiwamo Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) wanadaiwa Sh. bilioni 193.7.

Alisema pamoja na Tanesco kudai kiasi hicho cha fedha kwa wateja wake, kufikia Desemba 31, yenyewe ilikuwa inadaiwa na wazabuni Sh. bilioni 913.

"Kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilitenga Sh. bilioni 293.41 kwa ajili ya maendeleo ya Tanesco, lakini hadi Desemba 31 (nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18), shirika lilikuwa limepokea Sh. bilioni 42.1, sawa na asilimia 14 ya fedha zilizotengwa," alisema.

Ngalawa alisema kamati yake imebaini madeni ya Tanesco yanasababisha kuzorota kwa utendaji wa shirika na yamekuwa yakiongezeka na hakuna jitihada za serikali kusaidia kumaliza madeni hayo.

Alisema kamati yake pia imebaini Tanesco inaingia gharama kubwa za uzalishaji wa umeme kutokana na kutumia mafuta hasa kwenye maeneo ambayo hayajaunganishwa na gridi ya taifa.

Alisema hali ya upatikanaji wa umeme nchini bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo hasa Mkoa wa Dar es Salaam ambako nishati hiyo imekuwa si ya uhakika na kuathiri uchumi wa wananchi, akibainisha kuwa tatizo la miundombinu chakavu limechangia hali duni ya upatikanaji umeme wa uhakika nchini.

"Bunge linaishauri serikali kutenga na kupeleka fedha za kutosha kwa Tanesco kuiwezesha kuifanya matengenezo mitambo ya kufua umeme na miundombinu ya umeme nchini, hivyo kuepusha adha ya ukosefu wa umeme na kusababisha hasara kwa taifa," alisema.


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment