Tuesday, 6 February 2018

BUNGE LABAINI DOSARI SEKTA YA MADINI


BUNGE kwa mara nyingine limebainisha dosari zilizoikabili sekta ya madini nchini huku likiitaka serikali kuchukua hatua madhubuti kuzitatua.

Akiwasilisha bungeni mjini hapa jana, taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kwa kipindi cha Januari 2017 hadi Januari 2018, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratius Ngalawa, alibainisha kuwa serikali inamiliki mgodi mmoja tu kwa asilimia 100 ambao ni Mgodi wa Stamigold kupitia Stamico, ukiajiri zaidi ya Watanzania 700.

Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kumekuwa na jitihada ndogo za serikali katika kuusaidia kwenye masuala ya msingi kwa lengo la kuuendeleza.

Pia alisema kamati yake imebaini kuwa licha ya leseni zote za uchimbaji mkubwa na utafiti kukabidhiwa kwa Kampuni ya TANZAM 2000, hakuna kazi yoyote iliyokwishafanyika katika kuendeleza mgodi wa Buckreef ulioko mkoani Geita tangu kampuni hiyo iingie mkataba na Shirika la Madini (Stamico) mwaka 2011.

Alibainisha kuwa katika ubia huo, Stamico inamiliki asilimia 45 na TANZAM 2000 wenye jukumu la kutafuta fedha za kuendesha mgodi wana asilimia 55.

"Pamoja na kampuni kuripoti kuwa imekamilisha ufungaji wa mtambo mpya wa kuchenjua dhahabu, kamati inasikitishwa na kitendo cha mbia huyo kutozingatia ushauri wa Stamico kuhusu aina ya mtambo unaofaa kutumika katika eneo hilo," alisema na kuongeza:

"Kamati inaishauri serikali kuwa makini inapoingia ubia katika miradi ya sekta ya madini ili kuepuka wabia wa aina hii ambao hawazingatii ushauri wa mbia mwenza, jambo linalosababisha hasara zisizo za msingi."

Alisema kamati yake imesikitishwa na usimamizi mbovu wa Stamico katika mgodi huo licha ya kuwa na mashapo yenye uhakika wa kuzalisha dhahabu na kuliingizia taifa mapato.

"Ni mtazamo wa kamati kwamba, hatua zichukuliwe ili kurekebisha kasoro ambazo zimebainika katika ubia huo," Ngalawa alisema.

Alisema kamati yake inampongeza Rais John Magufuli kwa kuamua kujenga ukuta kuzunguka eneo la mgodi wa Mirerani mkoani Manyara ikiamini hatua hiyo itaongeza udhibiti wa biashara ya Tanzanite na kupunguza utoroshwaji wa madini hayo.

"Kamati inampongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wa kuigawa Wizara ya Nishati na Madini na kuwa wizara mbili tofauti. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa wizara hizi," alisema.

Alisema kamati yake pia inaunga mkono jitihada zinazoendelea za kushughulikia kwa kina mkataba baina ya Tanzanite One (T) Ltd na Stamico kwa kutumia sheria mpya ya rasilimali ambazo zinaruhusu kurejea makubaliano hasi katika mikataba ya ubia ili taifa linufaike na rasilimali zake.

Alisema moja ya dosari zilizomo katika mkataba huo ni kipengele kinachotamka kuwa faida itakayogawanywa kwa wabia itakuwa ni faida mabaki ambayo kimsingi tangu kuanza kwa mkataba huo Juni 20, 2013, faida hiyo haijawahi kupatikana kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.

Faida ya mabaki inapatikana baada ya kutoa gharama zote za uzalishaji na gharama zisizo za moja kwa moja kutoka katika mauzo.

GESI ASILIA

Kuhusu gesi asilia, Ngalawa alibainisha kuwa kamati yake haikuridhishwa na uhusiano wa ubia kuendeleza miradi ya gesi hiyo inayotekelezwa kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na PanAfrican Energy, Songas pamoja na Shirika la Umeme (Tanesco).

"Kamati iliona kuna haja ya Bunge kuingilia kati na kupata vyema ufafanuzi wa ziada kuweza kuishauri serikali juu ya mikataba na uhusiano baina ya wabia hao," alisema.

Alisema kamati yake inampongeza Spika Job Ndugai kwa kuunda kamati maalum iliyoshughulikia masuala ya maendeleo na matumizi ya sekta ya gesi asilia kwa lengo la kuongeza mapato nchini.

"Kupitia kamati hiyo, Bunge litaweza kuwa na uelewa wa kiwango cha juu na kupata namna bora zaidi ya kuishauri serikali katika sekta ya gesi," alisema.

Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo iliyoundwa Novemba 17 na kupewa kipindi cha mwezi mmoja kukamilisha kazi yake, bado haijawasilishwa bungeni.

Ngalawa alibainisha kuwa, kwa ujumla sekta ya madini imeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi hasa katika suala la ukusanyaji wa kodi za serikali.

Alisema sekta hiyo imekuwa ikichangia asilimia nne ya Pato la Taifa, mchango ambao ni kidogo kulinganishwa na ongezeko la uzalishaji katika sekta hiyo.


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment