Wednesday, 11 October 2017

MIAKA 30 JELA KWA WIZI WA KUTUMIA NGUVU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewahukumu watu wanne kwenda jela miaka 30 kila mmoja na kuchapwa viboko 12 baada ya kupatikana na hatia ya unyang'anyi wa mali ya zaidi ya Sh. milioni mbili.

Washtakiwa hao ni, Donald Nzwenka, Michael Paschal, Ally Akili maarufu kama Chinga na Kurwa Mwakagenda.

Hukumu hiyo ilitolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, baada ya kusikiliza mashahidi 15, wakiwamo 11 wa Jamhuri na wanne wa utetezi.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mwijage alisema mahakama yake imeridhika na ushahidi wa mashahidi wa utetezi bila kuacha shaka imewatia hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Akichambua ushahidi wa Jamhuri, alisema ni wajibu wa upande wa Jamhuri kuthibitisha kosa kwamba wakati wa ufanyaji wa tukio mtu alibeba kitu au kifaa cha hatari au walikuwa zaidi ya mmoja kuonyesha kuwa walitumia nguvu.

"Katika kesi hii mlalamikaji na mashahidi wengine wanaeleza kuwa Julai 7, 2013 majambazi walivunja mlango mkubwa wa nyumba yao kwa kutumia bomu na lilitambuliwa na polisi kuwa ni baruti," alisema.

"Majambazi hao waliingia na kuvamia katika chumba walichokuwa wamekaa kilichokuwa kinawaka taa. Ushahidi unaeleza mshtakiwa wa nne alishika panga na alianza kuwapiga na ubapa wa panga hilo na mashahidi walimtambua mshtakiwa,” alisema Hakimu wakati akiichambua hukumu hiyo.

Alifafanua kuwa siku ya tukio washtakiwa waliiba simu za mkononi nne zenye thamani ya Sh. milioni 1.3, fedha taslimu Sh.

150,000, cheni za dhahabu zenye thamani ya Sh. 750,000, vyote vikiwa na thamani ya Sh. 2,050,000  mali ya  Hobokela Mwakijambile.

Katika utetezi wao, washtakiwa waliokamatwa mahali tofauti, walidai kwa nyakati tofauti kwamba walipigwa wakiwa katika kituo cha polisi Oysterbay na kulazimishwa kuandika maelezo ya kukiri makosa.

"Utetezi wa aina hii hauaminiki na hauna uzito wa aina yoyote. Utetezi wa washtakiwa kwamba hawakushiriki katika kutenda kosa haukutikisa ushahidi wa Jamhuri. Washtakiwa walishiriki kutenda kosa na kwamba walitambuliwa ipasavyo," alisema.

"Nimeridhika na ushahidi wa Jamhuri, hivyo nawatia hatiani washtakiwa wote kama mlivyoshtakiwa kwa unyang'anyi wa kutumia silaha... Watakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 na watachapwa viboko sita wakati wa kuingia na vingine sita watakapomaliza kifungo chao," alisema Hakimu Mwijage.


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment