Saturday, 26 August 2017

NIYONZIMA - NIMETISHIWA KUUAWA

Kiungo wa kimataifa wa Klabu ya Simba Haruna Niyonzima.

Kiungo wa kimataifa wa Klabu ya Simba Haruna Niyonzima amefunguka na kudai haikuwa jambo rahisi yeye kuchukua maamuzi ya kuchezea Simba ila anamshukuru Mungu kwa kumtoa hofu ya kushambuliwa na kuuliwa na mashabiki wa Yanga wasiofahamu mchezo.

Niyonzima amezungumza hayo ikiwa zimepita siku chache tokea timu yake kuchukua ushindi wa kombe la Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya penati 5-4 iliyowakutanisha na watani wao wa jadi 'Yanga' na kusema alikuwa anawahofia sana mashabiki pengine wangeweza kumfanyia jambo lolote lile katika mchezo huo kwani ndiyo mchezo wake wa kwanza kucheza uso kwa uso na klabu yake ya awali.
"Nilikuwa na hofu na binadamu kwa kuwa niliishi na Yanga muda mrefu na timu ambayo kiukweli naiheshimu sana, nimeishi nao vizuri wala sikuwa na ugomvi nao kwa namna yoyote ile. Japo nilikuwa napata ujumbe 'message' nyingi za kunitisha na kuwatusi wazazi wangu pamoja na familia yangu kwa kuwa niliamua kuhamia klabu ya Simba", alisema Niyonzima.
Pamoja na hayo, Niyonzima aliendelea kwa kusema "kama mchezaji nilijaribu kuomba Mungu anipe moyo wa subira kwa sababu naamini sijafanya kibaya na wala sikumtusi mtu yoyote nilivyotoka Yanga baada ya kumaliza mkataba wangu 'so' haikuwa rahisi japokuwa mpaka leo hofu haijaisha vizuri kwa kuwa baadhi ya watu hawaelewi kama mimi natafuta maisha yangu pia inawezekana leo hii nipo hapa Simba halafu baadae nikawa pengine tena", alisisitiza Niyonzima.
Kwa upande mwingine, timu ya Simba leo inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na Ruvu Shooting FC katika mechi za kwanza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Saalam majira ya 10:00 jioni  kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.

No comments:

Post a Comment