Monday, 21 August 2017

MKAMATA MAGARI AGEUZIWA KIBAO

Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya

ZABUNI ya ukamataji wa magari yanayoegeshwa kimakosa katika Manispaa ya Moshi imegeuka ‘shubiri’ kwa wakala aliyepewa kazi hiyo, baada ya halmashauri kuruhusu wananchi wanaofungiwa vyuma au minyororo kwenye magari yao kukamata watumishi wake kwa uhalifu.

Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya, ametaka wakazi wake wasisite kuisaidia kampeni hiyo ya kukamata mawakala wanaoingia kwenye magari ya wananchi au kufunga vyuma kwenye matairi kwa kuwa huo ni ukiukwaji wa makubaliano ya mkataba.

Aliyazungumza hayo kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki, wakati akihutubia mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Jaffary Michael.

“Kuingia kwenye gari la mtu bila idhini yake au kufunga vyuma ama minyororo kwenye gari, huo ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine," alisema Mboya.

"Wananchi tusaidieni... mawakala wanaofanya hivyo wakamatwe na wafikishwe Polisi kwa hatua zaidi.”

Alisema atapeleka nakala iliyodurufiwa ya mkataba wa sasa Polisi pamoja na picha za mawakala na vitambulisho na kama mhusika hayupo katika orodha hiyo atafunguliwa mashtaka.

"Kwenye mkataba huu nitakuwa mkali," alisema zaidi Mboya. "Ni vizuri kampuni iliyopewa zabuni ya 'wrong parking' pamoja na wale wa kukusanya ushuru wa maegesho ya magari wakaheshimu mikataba yao maana sina urafiki na mtu anayekwenda kinyume.”


Chanzo - MuungwanaBlog

No comments:

Post a Comment