Saturday, 19 August 2017

58 MBARONI KWA MAUAJI WANAWAKE 5

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa

WANANCHI 58 wa kijiji cha Undomo, kata ya Uchama wilayani Nzega mkoani Tabora akiwemo diwani wa kata hiyo, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za mauaji ya wanawake watano wa kijiji hicho yaliyotokea wiki mbili zilizopita.


Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbrod Mtafungwa alisema watuhumiwa waliokamatwa ni wananchi, viongozi na diwani wanaoshikiliwa kwa tuhuma za kuwaua wanawake hao na kuteketeza miili yao kwa moto.
Alisema tukio hilo la kikatili lilitokea Julai 25 mwaka huu majira ya saa 12 za jioni ambapo inasemekana chanzo cha mauaji hayo ni imani potofu za kishirikina. Kamanda Mtafungwa aliongeza kuwa Julai 24, mwaka huu, majira ya saa mbili za usiku kijijini hapo binti wa darasa la tano wa shule ya msingi Undomo (jina limehifadhiwa) alionekana akichota mchanga na kuuweka katika kitambaa cheusi ndipo wananchi walimhoji kuhusu kitendo hicho naye akataja akinamama hao ambao kwa sasa ni marehemu kuwa ndio washirika wenzake katika uchawi.
Aidha, Kamanda Mtafungwa alibainisha kuwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea kufanywa na askari polisi na watuhumiwa wote watafi kishwa mahakamani Agosti 21, mwezi huu.
Wakati huo huo, Kamanda Mtafungwa alisema Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kukamata silaha 14 aina ya gobole, risasi 20 na ganda moja la risasi ya shortgun baada ya kutelekezwa na watu wasiojulikana kutokana na msako maalumu unaoendelea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mtafungwa alisema Agosti 15, 2017 majira ya saa 3:30 usiku katika kijiji cha Kabila kata ya Gongoni manispaa ya Tabora, Hassan Mkula miaka 55, mkazi wa Igosha aliuawa kwa kupigwa risasi ubavuni na kufariki papo hapo ambapo mwili wa marehemu ulionekana kuwa na matundu ya risasi na vipande vya risasi aina ya gobore.
Alisema katika tukio hilo ilikamatwa silaha moja aina ya gobore inayosadikiwa kuwa ya mtuhumiwa Ramadhani Mkula(28) aliyekuwa akiimiliki kinyume na sheria na aliitumia silaha hiyo kumua Hassan Mkula wakati watuhumiwa Halima Ramadhani ambaye ni mke wa marehemu, Ramadhan anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kuhusishea na kifo hicho.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment