Saturday, 19 August 2017

317 MBARONI KWA UHALIFU DAR

IGP Simon Sirro.
IGP Simon Sirro

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 317 kwa makosa mbalimbali ya kiuhalifu ikiwemo kukutwa na madawa ya kulevya.Kati ya watuhumia hao, watuhumiwa 150 wanashikiliwa kwa makosa ya kubugudhi abiria ikiwa ni pamoja na kuwaibia mali zao. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya alisema watuhumiwa hao wamekamatwa kufuatia operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na jeshi hilo.
Alisema makosa hayo ni kupatikana na madawa ya kulevya, unyang’anyi wa kutumia silaha, nguvu, utapeli, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kuuza pombe haramu ya gongo na kukutwa na bangi katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam.
Aidha, alisema katika operesheni hiyo ambayo ni endelevu jumla ya kete 96 za madawa ya kulevya zilikamatwa, huku puli zikiwa 87, misokoto ya bangi 107, pamoja na pombe haramu ya gongo lita 60.
“Oparesheni hii kali ya kuwasaka wahalifu wa makosa hayo mbalimbali ikiwemo kosa la kupatikana na madawa ya kulevya ni endelevu na hivyo raia wema wanaombwa kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwa Jeshi la Polisi ili kurahisisha kukamatwa kwa wahalifu hao na hatua kali za kisheria zifuate dhidi yao,” alisema Mkondya.
Akizungumzia watuhumiwa wa kubugudhi abiria na kuwaibia mali zao, Mkondya alisema jeshi hilo lilifanya misako na oparesheni kuanzia Agosti 14 mpaka Agosti 17, mwaka huu na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao katika stendi mbalimbali za mabasi.
Alisema Stendi ya Mabasi Ubungo walikamatwa watuhumiwa 39, Posta watuhumiwa 12, Feri watuhumiwa saba, Tegeta watuhumiwa 12, Tandika watuhumiwa 16, Mnazi Mmoja watuhumiwa sita, Kituo cha daladala Stesheni watuhumiwa watano, Temeke Sterio saba, Gerezani 16, Manzese watuhumiwa 12, Bunju B watuhumiwa wanane, Kijiwesamli watuhumiwa wawili na Buguruni watuhumiwa watatu.
Alisema katika mahojiano baadhi ya watuhumiwa hao walikiri kuhusika na matukio hayo na watuhumiwa wote watapelekwa mahakamani ili kujibu mashtaka yanayowakabili. Pia alisema tathimini iliyofanywa na jeshi hilo kabla na baada ya kufanyika kwa operesheni hiyo inaonesha matukio mengi ya kuibiwa na kubugudhi abiria yamepungua.
“Kabla ya kuanza operesheni tulipita kwenye vituo na tulibaini kuwa watu zaidi ya 102 walifika kwenye vituo mbalimbali vya Jiji kuripoti matukio kuanzia Agosti 7 hadi 11, lakini baada ya kuanza operesheni hii Agosti 14 hadi 17 wananchi 54 ndio walioripoti sasa utaona matukio yamepungua na tutaendelea mpaka tuone matukio yanayoripotiwa ni ziro,” alisema
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment