Sunday, 8 January 2017

ZITTO - SERIKALI IBORESHE SEKTA YA MADINI


KIONGOZI Chama cha ACT- Wazalendo Kabwe Zitto ameitaka serikali ihangaike na mabadiliko katika sekta ya madini ili kuisaidia nchi kunufaika na madini yaliyopo.
Zitto ametoa kauli hiyo wakati akimnadi mgombea wa ACT-Wazalendo, Ibrahim Masele, katika kampeni za uchaguzi mdogo katika kata ya Isagehe, Kahama Mjini.
Amesema, tangu Tanzania imeanza kuchimba dhahabu kwa kutumia kampuni kubwa ( uchimbaji mkubwa ) imeshauza nje dhahabu ya thamani zaidi ya sh trilioni 45 huku bajeti ya Tanzania ya mwaka huu 2016/17 ni sh 29 trilioni.
Hivyo alisema tangu mwaka 1997 uchimbaji mkubwa wa madini ulipoanza nchi imeuza madini nje lakini mauzo hayo ya nje hayafaidishi nchi.
“Kwa mauzo hayo na matrilioni hayo, Tanzania imepata dola milioni 800 tu kama mapato ya kodi na ushuru mbalimbali, sisi katika nchi licha ya kuuzwa kwa dhahabu zote tumepata trilioni moja na nusu tu kwa miaka yote, chini ya asilimia nne ya mapato yote ambayo kampuni za dhahabu zimeuza katika migodi yote,”aliongeza.
Kutokana na mazingira hayo aliwataka wananchi wa Isagehe kumchagua diwani wa ACT ili kuendeleza mapambano yatakayosaidia wananchi .
Alisema mwaka 2007, waliibua hoja ya ufisadi wa Mgodi wa Buzwagi, wakati huo ilikuwa kila mgodi kwenye mkataba unatoa dola 200,000 kwa mwaka kwenye halmashauri yenye mgodi kama mapato ya ndani.
Zitto alisema baada ya mapambano kuhusu Buzwagi iliundwa Kamati ya Bomani na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Dk Jakaya Kikwete na ilizalisha Sera mpya ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010 lakini licha ya kazi kubwa walioifanya wakati ule ya kuleta sera na sheria mpya ya madini lakini nchi bado hainufaiki na rasilimali hiyo.
Baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya sheria ya madini, Aprili 2010 ikaonekana kampuni zote zitalipa ushuru wa huduma asilimia 0.3, ya mapato ambayo kampuni inapata badala ya kulipa dola 200,000.
“Leo hii Kahama mnapokea zaidi ya dola za Marekani milioni 1.5 kwa mwaka. Nzega, Geita na Tarime nao wanafaidika na matunda ya kazi iliyoibuliwa na mbunge, sio wa chama tawala bali wa upinzani. Hii ndio faida ya mfumo wa vyama vingi na ndio maana nawasihi mumchague diwani kutoka upinzani hapa Isagehe ili kwenda kuongeza usimamizi wa fedha zenu kule baraza la madiwani,” aliongeza Zitto.
Alisema kutokana na historia hiyo anawakumbusha kuwakumbusha jambo ambalo walifanya pamoja na kuleta mabadiliko kwa watu wa Kahama na maeneo mengine yenye migodi ya dhahabu Kampeni za siasa zitahitimishwa Januari 21 mwaka huu kwa uchaguzi wa Mbunge kwa Jimbo la Dimani Zanzibar na katika kata 20 Tanzania Bara, utafanyika Januari 22 mwaka huu.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment