Friday, 6 January 2017

WAZIRI MAMBO YA NJE CHINA ZIARANI NCHINI

Balozi wa China nchini Tanzania, Dk LU Youqing (kulia) akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Shadrack Sagati (kushoto) na Rose Athumani ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza ilihusu ziara ya siku moja ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi anayetarajiwa kuwasili nchini Januari 19, mwaka huu. (Picha na Mroki Mroki).
Balozi wa China nchini Tanzania Dk. Lu Youqing (kulia) akizungumza katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari wa kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Shadrack Sagati (kushoto) na Rose Athumani ofisini kwake jijini Dar es Salaam. Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza ni kuhusu ziara ya siku moja ya waziri wa mambo ya nje wa China, Wang Yi anayetarajiwa kuwasili nchini Januari 19, mwaka huu.

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi atazuru nchini wiki ijayo kwa ziara ya kiserikali yenye lengo la kuendeleza urafiki uliopo kati ya nchi yake na Tanzania.
Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema jana kuwa balozi huyo anakuja nchini Jumatatu ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuzitembelea nchi kadhaa barani Afrika.
Alisema pamoja na mambo mengine, Wang atafanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi ambazo zina uhusiano mzuri na China jambo ambalo limevutia wawekezaji wengi kutoka China na kuifanya nchi yake kuwa wawekezaji wa pili ukiacha Uingereza.
Alisema kampuni za China ambazo zimewekeza nchini zimeajiri watu 150,000 katika sekta mbalimbali na zimetoa ajira ambazo sio za moja kwa moja zipatazo 350,000.
“Hii inadhihirisha kuwa nchi mbili hizi zina uhusiano wa karibu ya kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi,” alisema.
Waziri Wang anazuru Afrika kwa lengo la kusaidia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati Rais wa China Xi Jinping na viongozi wa Afrika pamoja na kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo na China. Pamoja na Tanzania, Waziri huyo atazuru Madagascar, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nigeria.
Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na waziri huyo kwa mwaka huu.
Alisema waziri huyo amechagua kuzuru Afrika kwa ziara ya kwanza ya mwaka kwa sababu umekuwa ni utamaduni wa wizara hiyo kwa miongo miwili sasa.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimefaidika na uhusiano na China katika maeneo ya kibiashara.
Alisema ziara hiyo ya siku moja itajikita zaidi kujadili namna ya kuboresha uhusiano katika maeneo ya kiuchumi na miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa Serikali ya China pamoja na utekelezaji wa makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa baina ya serikali za nchi hizo mbili.
Lu alisema Serikali ya China imekuwa inafadhili miradi mingi mkubwa inayofanywa na Serikali ya Tanzania ana akatoa mfano wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, ujenzi wa mkongo wa taifa pamoja na miradi mingine mingi ikiwemo ya uboreshaji wa nishati.
Kampuni ya China Power Investment (CPI) imewekeza katika Mradi wa Kuzalisha Megawati 300 za umeme ujulikanao kama Kinyerezi III. Nyingine, Poly Technologies inahusika katika Mradi wa Kinyerezi IV wa megawati 330 ambazo zinategemea kuongezeka hadi megawati 450.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment