Monday, 16 January 2017

MWILI WA MTANZANIA ALIYEFARIKI CHINA KULETWA KESHO KUTWA

MWANAFUNZI Mtanzania, Safina Msemo aliyekuwa akisoma shahada ya udaktari wa kutibu katika Chuo Kikuu cha Jiangxi, nchini China, amefariki dunia nchini humo na mwili wake unatarajiwa kusafirishwa keshokutwa kuja nchini kwa ajili ya maziko.
Mkurugenzi wa Global Education Link, Abdulmaliki Mollel, taasisi inayohusika na kuunganisha wanafunzi na vyuo nchi mbalimbali, alisema jana kuwa taratibu zote za kiserikali zilikamilika juzi Jumamosi ingawa haikuwa siku ya kazi.

“Tunaushukuru sana ubalozi wetu kwa sababu pamoja na kwamba ilikuwa siku ya mapumziko lakini hawakujali walitusaidia,” alisema.
Alisema mchakato unaofanywa kwa sasa nikusafirisha mwili na wamepata ndege ya Jumatano na gharama ni dola za Marekani 10,000 (Sh milioni 21).
Taarifa za awali zilidai kuwa, Msemo alifariki dunia Januari 13 mwaka huu.
Alijiunga na chuo hicho mwaka wa masomo 2015/2016 kwa ajili ya kozi ya awali na mwaka wa masomo 2016/2017 alijiunga na masomo ya shahada hiyo ya udaktari (MBBS).
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilidai kuwa, ripoti ya mwisho kutoka kwa daktari ya kiuchunguzi ilisema alikufa ghafla.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment