Monday, 16 January 2017

MSEKWA: WASOMI RUDHISHENI FADHILA KWA JAMII

SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amewakumbusha wasomi na watu wengine wenye uwezo wa kifedha kurudisha fadhila katika jamii zao.
Msekwa alitoa mwito huo jana wakati akikabidhi vitabu 1,246 vyenye thamani ya Sh milioni 9.8 katika shule ya sekondari Pius Msekwa iliyoko wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza.
Aidha, aliridhia sehemu ya vitabu hivyo ipelekwe kwenye shule nyingine za sekondari kama alivyoombwa na uongozi wa wilaya ya Ukerewe.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomiah Chang’ah, alisema shule nyingine pia zina upungufu wa vitabu na kuomba sehemu ya vitabu hivyo vipelekwe katika shule nyingine za sekondari ili kupunguza tatizo hilo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi vitabu kwa shule hiyo, ambayo mwaka huu imeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano, Msekwa alisema anapata faraja kuona hatua za maendeleo zilizofikiwa na shule hiyo aliyojenga kwa msaada wa marafi wa nje ya nchi mwaka 2009.
“Ndugu zangu hata mimi nilisomeshwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Kieshia baada ya baba yangu kufa hivyo niliguswa nikaona nijenge shule hii na kuikabidhi Serikali ili wanafunzi wengi wapate fursa ya kupata elimu,” alisema Msekwa.
Mke wa Msekwa, Anna Abdalla akizungumza katika hafla hiyo aliwataka wanafunzi wa kike waongeze bidii katika masomo kwa sababu taifa linahitaji wataalamu na viongozi wa nyadhifa kama alizopitia.
Anna aliyekuwa Mbunge kwa zaidi ya miaka 40 na kushika wadhifa wa Waziri na Mwenyekiti wa UWT Taifa, alisema kama angezembea katika masomo na kuwaza kuolewa asingefikia hatua hiyo.
Mkuu wa sekondari ya Pius Msekwa, Sudi Gewa, alisema katika shule hiyo vimebaki vitabu 671 na vingine vitapelekwa katika shule nyingine kama ilivyoelekezwa na mfadhili.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment