Monday, 16 January 2017

MFUMO WA KIELEKTRONIKI KUDHIBITI UTORO

KATIKA kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu nchini, Taasisi ya Econnect imetengeneza mfumo wa kielektroniki ambao utaisaidia kuimarisha mawasilianio kati ya utawala wa shule na wazazi au walezi.
Mfumo huo umejikita katika kutatua changamoto za upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati zinazohusisha idadi ya shule, idadi ya wanafunzi na idadi ya waalimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Hashim Magesa alisema mfumo huo pia utaisaidia serikali kutatua changamoto zinazolikabili Taifa hasa katika sekta ya elimu ikiwemo kudhibiti tatizo la utoro.

“Pamoja na tafiti kuonesha kwamba kuna changamoto za walimu kutofanya kazi ipasavyo na uwepo wa wanafunzi hewa, pia kuna changamoto ya utoro wa wanafunzi mashuleni ambapo wanafunzi wanaaga nyumbani wanaenda shuleni lakini hawafiki shuleni na kusubiri muda wa kurudi nyumbani ndio na wao pia hurudi nyumbani,” alisema.
Pia alisema mfumo huo utapunguza gharama za uendeshaji zisizo za lazima, kuboresha utendaji wa kazi kwa walimu kwa ujumla na kusaidia rasilimali fedha na rasilimali watu kupelekwa sehemu sahihi na kwa wakati sahihi.
Aidha alisema mfumo huo utasaidia serikali katika kupanga mipango ya maendeleo ya baadaye katika sekta ya elimu, kusaidia wadau mbalimbali wa elimu kuweza kujua kwa urahisi mahali shule inapatikana, mandhari yake, mawasiliano yake pamoja na historia fupi ya shule.
Alisema mfumo huo pia utawasaidia wadau mbalimbali wa elimu kupata nakala tofauti za vitabu pamoja na notisi kwa ajili ya kujisomea.
Alisema taasisi hiyo mara baada ya kukamilisha utengenezaji wa mfumo, iliomba ridhaa kutoka uongozi wa manispaa ya Ilala ili kukusanya takwimu katika shule zote za awali na msingi zilizopo ndani ya manispaa hiyo kwa ajili ya kujaribu ufanisi wa mfumo.
“Mara tu baada ya kupewa ridhaa na uongozi wa Manispaa ya Ilala, Taasisi ya Econnect ilianza kazi ya ukusanyaji takwimu na kuziingiza kwenye mfumo ambapo jumla ya shule 152 zikiwemo za serikali na za binafsi tulikusanya taarifa zake,” alisema.
Alisema taarifa walizokusanya ni pamoja na orodha ya wanafunzi kwa majina, jinsia, namba za simu za wazazi au walezi, idadi ya wanafunzi waliohama na kuhamia, idadi ya madawati au viti, orodha ya walimu kwa majina, jisnia, masomo anayofundisha, muda alioanza kazi, daraja lake kwa sasa, kiwango chake cha elimu, namba yake ya simu pamoja na kumpiga picha.
Taarifa nyingine walizokusanya katika shule hizo ni idadi ya walimu walihama au kuhamia, idadi ya walimu waliostaafu, idadi ya walimu walioko masomoni, idadi ya vyumba vya madarasa vilivyopo, mashimo ya vyoo na idadi ya kompyuta zilizopo, Magesa alisema serikali itakapouridhia mfumo huo, shule zitaunganishwa bure ila kwa wazazi watakaopenda kuutumia mfumo huo kwa hiari watachangia sh 300 kwa mwezi.
Hata hivyo, alipotafutwa, Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema alisema kuwa atafuatilia suala hilo.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Msongela Valela, aliahidi pia kutoa ufafanuzi leo.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment