Monday, 16 January 2017

HALMASHAURI ZAPEWA WIKI 2 ZINUNUE DAWA

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ametoa wiki mbili kwa Halmashauri zilizotumiwa fedha na serikali kwa ajili ya kununua dawa na hazijafanya hivyo, kuhakikisha zinanunua dawa hizo.
Jafo alizitaka halmashauri hizo hadi kufikia Januari 25, mwaka huu ziwe zimenunua dawa.
Ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, baada ya kuitembelea Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana na kuelezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk John Andrew kuwa fedha zinazotolewa na serikali kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali zimekuwa hazifiki kwa wakati hospitalini hapo.

Alisema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kupitia mfuko huo kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba, lakini fedha hizo kwa baadhi ya hospitali zimekuwa hazitumiwi ipasavyo na badala yake hurudishwa hazina wakati hospitali zikiwa na mahitaji makubwa ya dawa na vifaa vya tiba.
“Ifikapo Januari 25 mwaka huu halmashauri zote ambazo zimepokea fedha za ‘Basket Fund’ (Mfuko Mkuu wa Serikali) ziwe zimenunua dawa. Nataka wakuu wa wilaya na wabunge wawe wanapata taarifa ya ujio wa fedha za ‘basket fund’ ili waweze kusimamia”, alisema Jafo.
Alimtaka Dk Andrew kuhakikisha kuwa hospitali ina dawa za kutosha na kuonya kuwa hataki kusikia taarifa ya hospitali kukosa dawa.
Katika hatua nyingine, Jafo aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuendelea kutumia uadilifu katika ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kutoka mapato ya sasa ya Sh milioni 13 hadi kufikia Sh milioni 40.
Awali, Dk Andrew alisema kabla ya mfumo wa kieletroniki hospitali hiyo ilikuwa inakusanya milioni sita kwa mwezi lakini baada ya kutumia mfumo wa kieletroniki kwa sasa inakusanya Sh milioni 13 kwa mwezi.
Kwa upande wa vifaa vya tiba na dawa, Dk Andrew alisema katika kipindi cha Oktoba- Desemba mwaka jana, hospitali hiyo ilipokea dawa, vifaa vya tiba na vitendanishi vya maabara vya thamani ya Sh milioni 76 kutoka vyanzo vyake vya fedha.
Aliongeza kuwa hospitali imepeleka Sh milioni 38.5 kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kwa ajili ya kununua vifaa vya tiba na dawa kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment