Monday, 16 January 2017

BOTI YAUA MTOTO, 7 WANUSURIKA

BOTI ya utalii imepata ajali wilayani Mafia mkoani Pwani na kusababisha kifo cha mtoto wa miaka mitatu, wengine wawili wamepotea na saba wamenusurika.
Ajali hiyo imetokea zikiwa zimepita siku tano, tangu kutokea kwa ajali ya jahazi ya Mv Burudani katika Bahari ya Hindi mkoani Tanga na kusababisha watu 12 kupoteza maisha.
Boti hiyo ya utalii ikiwa na watu 10, ilipigwa na mawimbi na kuzama kwenye Bahari ya Hindi eneo la Kinaspa wilayani Mafia.
Ajali iliyotokea siku tano zilizopita ikihusisha jahazi namba Z5512 Mv Burudani katika bahari hiyo ya Hindi, pamoja na vifo 12, watu 33 walijeruhiwa.

Ilikuwa ikitokea Tanga kwenda Pemba na ilipinduka eneo la kisiwa cha Jambe kilichoko pwani ya bahari hiyo, kutokana na upepo mkali.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaib Nnunduma alisema kuwa watu hao walikuwa ni watalii kutoka Dar es Salaam wenye asili ya Asia.
Nnunduma alisema kuwa tukio hilo ni la juzi, Januari 14, saa 10 jioni baada ya injini moja kuzima kutokana na hali mbaya ya bahari na walipokuwa wakijaribu kuwasha injini nyingine ndipo walipopigwa na wimbi kubwa na boti hiyo kuzama.
“Hao walikuwa ni watalii wa ndani ambapo walikuwa kwenye eneo ambalo huwa wanafanya michezo ya baharini ambapo idadi yao ilikuwa watu tisa na waongozaji watatu na walikumbwa na tukio hilo wakati wanarudi, na kutokana mkondo mkali wa maji injini moja ikazima wakawa wanahangaika kuiwasha wimbi likaja likawapindua na kuwamwaga majini,” alisema Nnunduma.
Alisema kuwa wenzao ambao walikuwa nchi kavu walishikwa na wasiwasi kuona hadi jioni hawajarudi na ilitumwa boti kwenda kuangalia saa 3 usiku na kuwakuta wakiwa wanaelea huku wengine wakiwa wamepotea baharini na wakawaokoa watu saba watalii watatu wakubwa, watoto wanne na manahodha wawili.
“Hadi sasa watalii wawili hawajapatikana na nahodha mmoja aliokotwa ufukweni jana asubuhi akiwa hai ambapo aliogelea usiku kucha na kilichowasaidia wasizame ni makoti ya usalama ambapo mtoto mmoja alifariki,” alisema Nnunduma.
Alitoa mwito kwa kuwataka watu wanaotumia bahari kuwa na tahadhari kipindi hiki cha pepo za Kaskazi, kwani kuna upepo mkali wakati wakienda kwa ajili ya uvuvi au kuangalia samaki wakubwa.
Mmoja wa wavuvi alisema kuwa watalii wamekuwa wakienda kwenye eneo hilo kwani kuna uoto wa asili wa bahari chini ambapo kuna samaki wengi na majani na samaki huzaana watalii huwa wanakwenda kwa ajili ya kuzamia chini. Alisema kuwa mtoto aliyekufa alibebwa na nahodha mmoja wapo na aliogelea naye kwa muda mrefu tangu boti ilipozama lakini alichoka.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment