Monday, 16 January 2017

ACT-WAZALENDO WAMKUBALI MAGUFULI


CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kinaunga mkono kazi zinazofanywa na Rais John Magufuli pamoja na serikali yake kwa sababu kuna mambo mazuri yanafanyika.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni za udiwani jana, katika kata ya Kijichi Dar es Salaam, Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto alisema hawajutii kumuunga mkono Rais Magufuli.
Katika mkutano huo, Zitto amewaomba pia wananchi wa Kijichi kumchagua mgombea udiwani wa chama hicho, Edgar Mkosamali katika uchaguzi utakaofanyika Januari 22 mwaka huu.

“Sisi kama chama, ACT Wazalendo tulimuunga mkono Rais tangu mwanzo wa utawala wake na kumkabidhi Ilani ya uchaguzi ya chama chetu kama ishara ya kwamba uchaguzi umekwisha na sasa tujenge nchi yetu. Hatujutii kumuunga mkono kwa sababu kuna mambo mazuri amefanya kuhusu nchi yetu,” alisema Zitto.
Zitto alizitaja kazi ambazo chama chake kinaunga mkono rais kuwa ni pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi nchini.
“Ameondoa hali ya ‘impunity’ iliyokuwa imeshika mizizi nchini na kuwawajibisha watendaji na waziri aliyekiuka maadili ya kazi”.
Hata hivyo, Zitto alisema chama chake kinamuomba Rais Magufuli na serikali yake kuwa wasikivu katika matatizo yanayowakumba watanzania, ikiwa ni pamoja na upugufu wa chakula nchini jambo ambalo hivi karibuni alilizungumza na kusema kuwa nchi haina njaa na kwamba hayuko tayari kugawa chakula.
Zitto alisema suala hilo limekuwa ni ajenda ya taifa ambapo amewapongeza pia viongozi wa dini kwa kutoa matamko ya kuhamasisha Watanzania kuliombea taifa kuepuka baa la njaa.
Alisema Rais anafanya kazi kwa mujibu wa Katiba ya nchi na Katiba imetoa wajibu wa lazima kwa serikali kulinda watu pale ambapo yanatokea majanga ambayo yanawazidi wananchi.
Alitoa mwito kwa Watanzania kuweka rekodi ya hali ya chakula na takwimu ya maafa yoyote yanayotokana na njaa, ili Rais awajibishwe kwani alisema hayuko tayari kutoa chakula kwa wananchi.
Rais Magufuli hivi karibuni, akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Somanda, Bariadi, mkoani Shinyanga, alisema kuwa serikali haitatoa chakula cha msaada kwa wananchi na kuhimiza wananchi kulima na kujituma.
Kabla ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, Zitto alikaririwa akiitaka serikali itangaze rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria.
Chanzo - HabariLeo

No comments:

Post a Comment